Google PlusRSS FeedEmail

MAKALA



Upotoshaji na chuki kwa Rais, CCM havitaubadilisha ukweli

Na Charles Charles

KUPITIA makala yake iliyokuwa na kichwa kinachosema: “Ni wazi kuwa Chama legelege
huzaa Serikali legelege”, mwandishi mmoja wa habari, Jumatano wiki hii, alionyesha kiasi
gani anavyomchukia Rais Jakaya Kikwete, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake!

Alionyesha chuki zake hizo akiwapotosha wasomaji wake, lakini kwa sababu ni mzoefu na 
asiyekuwa tayari kukubaliana na ukweli hata kama akiambiwa kirafiki sana, nimelazimika 
kumjibu uongo wake huo kwa njia ileile aliyotumia yeye kuwadanganya Watanzania.

Nimewahi kuwasiliana naye kwa kutumia simu yangu ya mkononi, kumwambia alivyokuwa 
akipotosha katika makala zake nyingine, lakini hakujibu kwa sababu inawezekana kwamba
 analenga kuichafua CCM kutokana na chuki zake za kisiasa.

Ndiyo maana Jumatano wiki hii, katika mwendelezo wake huo aliandika makala nyingine ili
 pamoja na mambo mengine, kumpaka matope Rais Kikwete akiamini falsafa kuwa “kalamu
 inaua kwa haraka kuliko risasi”.

Alikuwa akiizungumzia ripoti iliyotolewa mwezi uliopita na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa 
Hesabu za Serikali, Ludovick Uttoh, na kuitumia kwa makusudi, ‘kumchafua’ Rais Kikwete
 huku akidai kuwa hayo “ni matunda ya serikali iliyozaliwa na chama legelege”.

“Kamati Kuu ya CCM ilikutana Ikulu, Dar es Salaam na kumshauri Rais Jakaya Kikwete
 kuwaondoa Mawaziri wabovu. Kitu kimoja ambacho hadi sasa sijakielewa ni kwamba, hivi
 alikuwa anasubiri ushauri wa Kamati Kuu ya Chama chake ndipo awawajibishe Mawaziri wanaotuhumiwa (kwa ubadhirifu na ripoti ya CAG).

“Nasema hivyo kwa sababu, kabla Rais Kikwete hajaanza safari ya Brazil, ripoti ya CAG
 ilikuwa tayari na pengine alishapelekewa”, anaandika katika makala yake hiyo na kuendelea:


“Lakini wakati anasafiri, huku nyuma CAG akatoa ripoti ya aibu kwa serikali ambayo Waziri
 Mkuu, Mizengo Pinda alishindwa kuitolea uamuzi. Hata katika hotuba yake ya kuahirisha 
bunge hakuzungumza lolote kuhusu kuwawajibisha mawaziri wanaotuhumiwa”.

Mbali na hayo, mwandishi huyo anasema kwamba aliporejea nchini, Rais Kikwete alisafiri 
tena, safari hii akienda kwenye mazishi ya aliyekuwa Rais wa Malawi, Bingu wa Mutharika,
 halafu aliporudi akakuta kuna sherehe za Muungano.

“Wakati wote huo, Watanzania (walikuwa) wanamsubiri yeye ili aje ategue kitendawili cha 
Baraza la Mawaziri”, anasema na kuongeza:

“Hapo ndipo Kamati Kuu ya CCM ilipokutana Ikulu ili kumshauri Rais eti awawajibishe 
Mawaziri. Pamoja na ukweli kwamba CCM imeunda serikali, hivi kweli Rais anasubiri 
ushauri wa kuwawajibisha watu wanaothibitika kutenda uhalifu?”

Huyo ndiye mwandishi wa makala anayejaribu kwa maarifa yake yote, kuonyesha chuki
 zake za wazi dhidi ya Rais Kikwete, CCM na serikali katika ujumla wake wote.

Anafikia hatua ya kutumia nafasi anayopata katika chombo hicho cha habari kuwapotosha
 kwa makusudi wasomaji wake. Anataka akidhi matakwa yake dhidi ya pande hizo ikiwemo kuzichonganisha kwa watu ili pengine afikie lengo lake hapobaadaye.

Anafanya hivyo akitumia kichaka kilichoanza kuchakaa cha waandishi wa habari wanaodai  hawafungamani na upande wowote, lakini idadi kubwa kati yaondio vinara wa uchochezi, 
uzushi, fitina, uongo na majungu dhidi ya CCM na serikali yake.

Ni vigumu kusema mwandishi huyo eti hafungamani na upande wowote kisiasa hata kama
hasemi hadharani, lakini haiwezekani iwe hivyo kwake isipokuwa vinginevyo.

Ni uzushi mkubwa kudai kuwa Kamati Kuu ya CCM ndiyo ilimshauri Rais Kikwete eti
 awawajibishe Mawaziri waliotajwa na ripoti ya CAG, na pia ni uongo kusema watendaji
hao tayari wamethibitika kwamba wametenda uhalifu wa jinai bali bado ni watuhumiwa.

Kwanza nataka mwandishi huyo ajue kuwa safari au ziara za Rais, Makamu wa Rais ama 
Waziri Mkuu siyo za kupanga leo na kuondoka kesho kamazilivyo zake, badala yake zote
 – isipokuwa za dharura kamavile misiba au majanga – huwepo kwa muda mrefu, nyingine
 hadi nusu mwaka mbele na hata zaidi ya hapo.  

Katika hali hiyo, ziara aliyoifanya Rais Kikwete huko Brazilakianzia Brasilia, mji mkuu wa
 nchi hiyo haikuwa ya ghafla bali ilipangwa zaidi ya miezi sita kabla ya kuanza kwake, na pia
 mkutano aliohudhuria kule Rio de Janeiro, haukupangwa wakati mkutano wa saba wa Bunge
 la Jamhuri ya Muungano ukianza mjini Dodoma. Ulipangwa zaidi ya miaka miwili iliyopita.

Aidha, kifo cha Mutharika hakikupangwa kwa namna zote na Rais Kikwete katika upande 
wa kwanza, na pili mazishi yake yalipangwa na serikali ya Malawi na familia ya marehemu, 
hivyo yasingeahirishwa hadi siku nyingine kutokana na dharura aliyopata Rais wa Tanzania
 na hata vinginevyo.

Mbali na safari hizo, sherehe za Muungano kamwe siyo tukio linaloweza kuahirishwa wala
 kusogezwa mbele hata kwa siku moja tu, halafu mgeni wake rasmi hawezi kuwa mwingine 
isipokuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye sasa ni Jakaya Kikwete.

Kutokana na hali hiyo katika namna zote, ziara yake Brazilpamoja na safari aliyokwenda
 kwenye mazishi ya Mutharika huko Malawi asingeweza kuziahirisha hata iweje, halafu
 ilikuwa haiwezekani kwake kutokuwa mgeni rasmi katika Sherehe za Muungano, Alhamisi
 ya wiki iliyopita, wakati yupo nchini na siyo mgonjwa mahututi isipokuwa bukheri wa afya.

Inawezekana mwandishi wa makala hiyo hajui chochote kuhusiana na ukweli huo, lakini pia
 huenda ana mkakati maalum wa ‘kumchafua’ mkuu huyo wa nchi kwa sababu za kisiasa na
 hata vinginevyo.

Pamoja na uchovu wa safari ndefu alizofanya bila kupumzika: kwanza akitoka Brazil hadi
 Marekani alikobadilisha ndege, akarudi Tanzania kupitia Ulaya na kesho yake asubuhi tu 
akasafiri kuelekea Malawi, akarudi usiku kutoka huko na asubuhi akaamkia kwenye sherehe
 za Muungano katika Uwanja wa Uhuru hata kama angekuwa Mtume wa Mungu angechoka 
akilini na kimwili, hivyo anachopaswa ni kupongezwa na si kubezwa kwa chuki za namna 
zote.

Kana kwamba haitoshi, kutoka huko ambako aliongoza sherehe za miaka 48 ya Muungano
 wa Tanzania Bara na Zanzibaralielekea moja kwa moja ofisini kwake, Ikulu, na kukutana 
faragha – tena kwa muda mrefi – na Waziri Mkuu wa nchi hii, Mizengo Pinda.

Ni kupitia kikao hicho cha dharura ndipo alipopewa taarifa rasmi ya kile kilichojiri katika
 mkutano wa saba wa bunge, Dodoma, uliokuwa umemalizika takribani siku tatu tu kabla 
ya hapo na kuitolea uamuzi wa papo hapo.

Akaita kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya CCM, kesho yake tu, ili aiambie uamuzi
wa haraka aliofikia wa “kulisuka upya” Baraza la Mawaziri, hivyo ilichofanya yenyewe
ni kumuunga mkono pekee, basi.

Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam, siku ileile, Katibu
wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye hakusema kuwa 
Kamati Kuu ya CCM ndiyo ilimuita ili imshauri kufanya hivyo isipokuwa ilipokea taarifa 
yake tu.

Aliamua kufanya hivyo mwenyewe akianza na Mawaziri, kisha watafuatia watendaji wote
 wa idara na taasisi za serikali waliotajwa katika ripoti hiyo ya CAG, kwamba wanahusika
 kwa namna moja ama nyingine na ubadhirifu wa fedha hizo za umma.

“Kamati Kuu imeridhika na imebariki uamuzi wa Rais wa kulisuka upya Baraza la Mawaziri
 na taasisi nyingine zilizoainishwa katika ripoti ya CAG”, alisema Nape, kauli ambayo hata
 hivyo inapotoshwa kwa makusudi na baadhi ya waandishi wa habari kutokana na chuki 
zao kwa Rais, CCM na serikali yake.

Wanadai alishauriwa kufanya hivyo na Kamati Kuu ya CCM kinyume cha ukweli, lengo 
ni kutaka ionekane kamwe asingefanya kitu chochote bila kushauriwa, uongo ambao uko
 wazi hadi kwa mtu aliyekosa hata elimu ya chekechea.

Akigusia uzushi huo dhidi yake kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, Jumanne 
wiki hii, Rais Kikwete alisema kwamba yamezungumzwa mengi huku mengine yakikolezwa.

“Mara Kikwete ampinga Pinda, mara nimepanda ndege kwenda Dodoma. Mengine
 (kati yake) yamesemwa ya kweli, mengine yameongezewa na mengine ni ya uongo kabisa”,
 alisema, ukweli ambao uliendelea tena kuonekana kesho yake, Jumatano, ikiwemo makala
 ya mwandishi huyo wa habari.

Mbali na uongo kwamba alishauriwa na Kamati Kuu “kulisuka upya” Baraza la Mawaziri,
 Rais Kikwete pia alifichua kuwa hata kujadiliwa bungeni kwa ripoti hiyo ya CAG ilikuwa  
matakwa yake mwenyewe.

“Mimi ndiye niliamua ripoti hii ijadiliwe kwa uwazi bungeni…Nilifikia uamuzi huo baada ya
 kuona wapo baadhi ya watu ambao ni mchwa wanaokula fedha za umma”, alisema katika 
hotuba hiyo ya Mei Mosi alikokuwa mgeni rasmi.

Hivyo ndivyo Rais anavyotungiwa uzushi na baadhi ya watu. Anazushiwa uongo kwamba
 hawezi kuwaondoa Mawaziri mpaka eti ashauriwe na Kamati Kuu ya CCM.

Anaambiwa kwamba alikwenda Brazil, halafu aliporudi akasafiri tena kuhudhuria mazishi ya
 Mutharika, kisha akaenda kwenye sherehe za Muungano badala ya kushughulikia ripoti ile
 ya CAG huku wananchi wakisubiri ategue kitendawili hicho ambacho kiuhalisi hakipo
 isipokuwa majungu, umbeya, uzabina na uzandiki wa mawazo.

Pamoja na kusingiziwa kwa hasira na wivu wote wa kisiasa kutoka kila pembe ya nchi hii,
 upotoshaji na chuki zote hizo kwake na chama chake haviwezi kubadilisha ukweli wowote.

Wale wanaoimba kuwa CCM ni legelege watapayuka mpaka midomo yaoipasuke, kisha watasambaratika kama kishada kilichokwenda harijojo na kuiacha ikiwa palepale, vilevile
na ileile!

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Msaidizi, Idara ya Siasa na Uhusiano wa 
Kimataifa ya CCM. Anapatikana kwa Simu Na. 0713 676 000 na 0762 633 244

This entry was posted in

Leave a Reply