Google PlusRSS FeedEmail

ASILI YA MFUMO WA SERIKALI MBILI - JULIUS K. NYERERE.

Mwalimu Julius K. Nyerere


Nchi mbili zinapoungana na kuwa nchi moja mifumo ya kawaida ya katiba ni miwili;
Muungano wa serikali moja, au shirikisho la serikali tatu. Kwa mfumo wa kwanza kila nchi itafuta serikali yake,na nchi mpya inayozaliwa itakuwa ni nchi moja yenye serikali moja. Katika mfumo wa pili kila nchi itajivua madaraka Fulani ambayo yatashikwa na serikali ya shirikisho na itakuwa na serikali ambayo itakuwa na mamlaka juu ya mambo yaliyobaki.
Mambo yatakayoshikwa na serikali ya shirikisho ni yale ambayo yakibaki katika mamlaka ya nchi zilizoungana, basi kwa kweli nchi hizo zitakuwa hazikuungana kuwa nchi moja, basi zinaendelea kuwa nchi mbili zenye ushirikiano mkubwa katika mambo Fulani Fulani. Nchi za Afrika Mashariki zilikuwa katika hali kama hiyo kabla ya kuvunjika kwa jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Zilikuwa ni nchi tatu zenye ushirikiano mkubwa, lakini hazikuwa nchi tatu zilizoungana kuwa Nchi moja yenye muundo wa shirikisho. Shirikisho halisi la nchi mbili litakuwa ni nchi moja yenye serikali tatu, serikali ya shirikisho, na serikali mbili za zile nchi mbili za awali zilizoungana kuzaa nchi mpya moja.

Tanganyika na zanzibar zilipoamua kuungana na kuwa Nchi moja, tungeweza kufuata mmojawapo wa mifumo hiyo ya kawaida. Lakini tulishindwa kufanya hivyo kwa sababu ya udogo wa Zanzibar na ukubwa wa Tanganyika. Zanzibar ilikuwa ina watu laki tatu (300,000) na Tanganyika watu milioni kumi na mbili (12,000,000).

Muungano wa serikali moja ungefanya ionekane kama Tanganyika imeimeza Zanzibar. Tulikuwa tunapigania Uhuru na Umoja wa Afrika; hatukutaka tudhaniwe, hata kwa makosa, kwamba tunaanzisha ubeberu mpya! Kwa hiyo mimi nilipinga mfumo wa serikali Moja na Shirikisho la serikali tatu lingekuwa ni gharama kubwa mno kwa Tanganyika. Zanzibar ingeendesha  serikali yake na kuchangia gharama za kuendesha serikali ya shirikisho; na Tanganyika ingefanya vivyo hivyo. Lakini ni dhahiri kwamba mchango wa Tanganyika ndio hasa ungeendesha serikali ya shirikisho.
 Kwa hiyo Tanganyika ingeendesha serikali yake ya watu 12,000,000 na pia ndiyo ingetoa sehemu kubwa ya kuendesha serikali ya shirikisho la watu 12,300,000. Ni watu wanaofikiri kwa ndimi zao wanaodhani kuwa gharama ya serikali yoyote kati ya hizo ingekuwa ndogo. Gharama ya serikali ya Tanganyika isingekuwa ndogo, (waulizeni wazanzibari) na wala ya serikali ya shirikisho isingekuwa ndogo, hata bila gharama za mambo yasiyo ya shirikisho. Na gharama zote hizo kwa kweli zingebebwa na Tanganyika.

Kwa hiyo ilitupasa tujiulize kwa nini tunataka kuibebesha Tanganyika gharama zote hizo; na hasa kwa nini tunataka Serikali  ya Tanganyika? Hivi tuna hofu ya kwamba Tanganyika, bila kuwa na serikali yake, itaonekana kuwa imemezwa na Zanzibar? Hofu yetu ni kwamba tukiwa na serikali moja Tanganyika itaonekana kuwa imeimeza Zanzibar. Basi na tutafute muundo ambao utaiondolea Zanzibar hofu hii ya kumezwa, bila kuibebesha Tanganyika mzigo wa kuendesha serikali mbili zenye uzito unaolingana.

Hivyo ndivyo tulivyofanya, na hiyo ndiyo asili ya muundo wa muungano wa serikali mbili. Badala ya kutungua mfumo uliopo kama wapumbavu, tulitazama hali halisi yetu ilivyokuwa, na tukabuni mfumo utakaotufaa zaidi.


Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume wakisaini Hati ya Muungano.


This entry was posted in

Leave a Reply