Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilson Mukama, ameagiza majengo yaliyovunjwa wakati wa maboresho ya Chuo Cha Kilimo na Ufundi cha Kaole, Bagamoyo mkoa wa Pwani, yajengwe tena na kuwa katika muonekano wake wa awali ili kuhifadhi historia ya harakati za ukombozi Barani Afrika.
Ameagiza pia kupitiwa upya mkataba kati ya Jumuiya ya Wazazi Tanzania na mwekezaji ili kuhakikisha kuwa hakuna mkanganyiko unaojitokeza katika usimamizi na pia kuainisha wazi namna majengo hayo ya kihistoria katika eneo hilo yatakavyotunzwa.
Mukama ametoa maagizo hayo wakati alipozungumza na mwekezaji wa mradi wa chuo hicho, Julian Bujugo na uongozi wa Jumuiya ya Wazazi inayomiliki eneo hilo, baada ya kufanya ukaguzi na kushuhudia majengo matatu yaliyokuwa yakitumiwa na Wapigania Uhuru wa Chama Cha FRELIMO cha Msumbiji yakiwa yamebomolewa.
Majengo yaliyobomolewa ni pamoja na ukumbi uliokuwa ukitumiwa kufanyia mikutano na wapigania ukombozi, banda la mlinzi na ghala la kuhifadhia vifaa mbalimbali wakati huo.
FRELIMO ilikabidhi majengo yote katika eneo hilo kwa CCM baada ya Msumbiji kupata uhuru wake mwaka 1975 ambapo baadaye CCM nayo iliyakabidhi kwa Jumuiya yake ya Wazazi, kwa ajili ya kuanzisha mradi wa shule ya sekondari.
Upande wa majengo yaliyovunjwa, Mukama alisema, ni lazima yajengwe tena pale pale yalipokuwa na yawe na muonekano ule wa zamani hata kama yataboreshwa lakini yasipoteze uhalisia wake.
"Majengo haya ni kumbu kumbu muhimu ya harakati za ukombozi barani Afrika, haifai kuyabomoa kwa kisingizio chochote, ninaagiza walioyabomoa wayajenge kama yalivyokuwa kwa sababu yataendelea kuwa heshima kwetu", alisema Mukama.
Alimtaka msimamizi wa Chuo hicho kuhakikisha katika kuboresha majengo yote katika eneo hilo, ayafanye kuwa na muonekano mzuri tu, lakini asiyabadilishe muundo wala muonekano wake.
Kuhusu mkataba, Mukama alisema, ili majengo na masuala mengine yote yaweze kuwa na udhibiti wa uhakika ni lazima upitiwe upya ili usizuke mgogoro baadae wa nani ni nani katika umiliki, kwa sababu licha ya mwendelezaji kubadili kutoka shule ya sekondari na kuwa chuo bado mmiliki halali ni Jumuia ya Wazazi.
Katika mazungumzo, baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Wazazi waliofuatana na Katibu Mkuu wa Jumuia hiyo, Suleiman Dadi, walionyesha wasi wasi wao ikiwa mwendeshaji huyo anafanya mambo yake kwa sasa kwa mujibu wa mkataba.
"Hadi sasa tunaona hapa sasa ni Chuo badala ya sekondari lakini hatujajua msimamizi halisi ni nani, maana tukija hapa Mwendeshaji (Bujugo) anasema hatutambui, wakati sisi ndiyo viongozi wa Jumuia hii hapa wilaya ya Bagamoyo", alisema Mwenyekiti wa Wazazi wilaya hiyo, Kasim Gogo.
Katika hatua nyingine, Katibu Mukama ameutaka uongozi wa Chuo hicho kuacha kufanya biashara ya kuuza pombe na nyama ya nguruwe kwenye eneo la chuo hicho kwa sababu kufanya hivyo si sahihi kwenye chuo kwa kuwa wanaosoma eneo hilo wengi bado ni vijana wadogo.
"Hili la kuuza pombe hapa, na kitimoto, halikubaliki, vijana wanaosoma hapa wengi bado ni wadogo, sasa kuweka pombe katika eneo la chuo namna hii mtawaharibu, baa ifungwe mara moja", alisema Mukama.
Mapema Mukama alitembelea maeneo ya chuo hicho na kushuhudia ukarabati mkubwa ukifanyika, ikiwemo kujenga upya madarasa na vyoo na baadhi ya majengo yakiwa tayari yamebomolewa kwa ajili ya kujengwa mapya.