Rais Dk. Jakaya Kikwete |
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania,
Ndugu Ayoub Omari Juma;
Waziri wa Kazi na Ajira -Mheshimiwa Gaudensia Kabaka (MB);
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mheshimiwa Chiku Galawa;
Waheshimiwa Mawaziri na Wabunge;
Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Dunia (ILO) Kanda ya
Afrika Mashariki, Ndugu Alexio Musindo;
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi,
Ndugu Nicholaus Mgaya;
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE),
Dr. Aggrey Mlimuka;
Waheshimiwa Mabalozi;
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi;
Wenyeviti na Makatibu wa Vyama vya Wafanyakazi;
Viongozi wa Serikali;
Wawakilishi wa Vyama vya Siasa;
Ndugu Wafanyakazi na Wananchi;
Mabibi na Mabwana.
Shukrani
Nakushukuru Ndugu Ayoub Omari Juma na viongozi wenzako wa TUCTA kwa fursa ya kuungana na wafanyakazi wenzangu kusherehekea sikukuu ya wafanyakazi duniani mwaka huu. Naungana nanyi kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, aliyetujaalia uhai na afya, na kutuwezesha kukutana leo katika sherehe hizi, hapa Tanga.
Nawapongeza viongozi wa Mkoa wa Tanga wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Chiku Galawa na wakazi wote wa Mkoa huu, kwa kukubali kuwa wenyeji wa sherehe hizi na tunawashukuru kwa kutupokea vizuri. Aidha, nawapongeza sana kwa maandalizi mazuri mliyoyafanya kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyakazi wa Mashambani (TPAWU), TUCTA na Wizara ya Kazi na Ajira. Aidha, kwa namna ya pekee nawapongeza wafanyakazi na wananchi wote mliokusanyika hapa leo kuadhimisha siku hii muhimu kwetu sote.
Pongezi kwa Wafanyakazi Bora
Ndugu Wananchi;
Kama ilivyo utamaduni wa sherehe hizi, leo tena nimetunuku tuzo kwa wafanyakazi bora wa mwaka huu. Wenzetu hawa wanastahili pongezi zetu sote kwa kufanya kazi kwa bidii, maarifa na nidhamu. Nawomba waendelee na moyo huo ili hata mwakani watunukiwe tena. Nchi yetu itajengwa na watu kama hawa wanaojituma na kufanya kazi kwa bidii, ufanisi na nidhamu. Kwa wale ambao hawakupata safari hii, nawaomba wasikate tamaa bali wachukulie kupata kwa wenzao leo kama chachu na motisha kwao kuongeza bidii zaidi kazini ili mwakani nao watambuliwe na kuzawadiwa.
Kauli Mbiu ya Mwaka Huu
Ndugu Rais wa TUCTA;
Ndugu wafanyakazi;
Nimesikiliza risala yenu iliyowasilishwa kwa ufasaha na Katibu Mkuu Ndugu Nicholaus Mgaya. Mambo mliyoyataja ni ya msingi kwa maslahi na ustawi wa wafanyakazi na taifa letu. Risala yenu nimeipenda kwa vile kwa kila suala mlilolizungumza mmetoa mapendekezo ya jinsi ya kulitatua. Napenda kuwaahidi kuwa tumesikia na tutayafanyia kazi. Inawezekana tusifikie pale mnapopataka mara moja lakini tutafika muda si mrefu.
Kauli Mbiu yenu inayosema, “Mshahara mdogo, kodi kubwa na mfumuko wa bei, pigo kwa mfanyakazi’’ ni kauli muafaka kabisa. Inaeleza ukweli wa mambo ulivyo na kilio cha wafanyakazi nchini. Narudia kuwahakikishieni kuwa mimi na wenzangu Serikalini tunazitambua changamoto zinazowakabili wafanyakazi na kuzitafutia jawabu ndiyo shughuli tuifanyayo kila siku. Ninyi na mimi ni mashahidi kwa namna gani Serikali yetu inavyojitahidi kushughulikia masuala yahusuyo haki na maslahi ya wafanyakazi nchini. Mambo mengi yamefanyika yanayoelezea uthabiti wa dhamira ya Serikali.
Ndugu Rais wa TUCTA na Ndugu Wafanyakazi;
Miongoni mwa mambo ambayo yamefanyika ni pamoja na: Kutungwa kwa Sera mpya ya malipo ya mishahara na motisha katika utumishi wa umma; kuundwa kwa Bodi ya Mishahara katika utumishi wa umma; kutunga Sheria na kuanzishwa kwa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii; kupunguza kodi ya mapato kwenye mishahara; kuongeza kiwango cha chini cha kutoza kodi ya mapato na kuweka utaratibu wa kupanga kima cha chini cha mishahara katika sekta binafsi kwa kuzingatia tija ya kila sekta.
Ndugu Wafanyakazi;
Naamini nanyi mnajua kwamba wapo waajiri wengi wanaotulaumu kuwapa wafanyakazi haki na ulinzi mkubwa dhidi ya waajiri, lakini hatutishiki wala kubabaika na hivyo hatutaacha kupigania haki za wafanyakazi kama tufanyavyo kwa haki za waajiri. Nchi yetu ni miongoni mwa nchi za mwanzo kutia saini Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Wafanyakazi wa Majumbani. Kwa miaka nenda rudi, ndugu zetu hawa wamekuwa wakikandamizwa kupita kiasi. Kilio chao tumekisikia na tumeamua kuchukua hatua za kuwakomboa.
Mshahara Mdogo
Ndugu Wafanyakazi;
Chama kinachounda Serikali hii kina historia ya kipekee na wafanyakazi tangu enzi za kupigania uhuru na baada ya uhuru. Hatuwezi na wala hatuthubutu, hata siku moja, kuwatelekeza wafanyakazi. Mtakumbuka kuwa katika hotuba yangu ya Mei Mosi Mwaka jana (2011) pale Morogoro nilisema kuwa Serikali inatambua kilio cha wafanyakazi wake kuhusu maslahi. Niliwaelezea hatua mbalimbali ambazo Serikali imekuwa inazichukua kuboresha maslahi ya wafanyakazi. Niliwahakikishia wafanyakazi wa nchi yetu kwamba, hakuna upungufu wa dhamira wala utashi wa kisiasa wa kuboresha maslahi yao kwa upande wangu binafsi au wa wenzangu Serikalini. Uwezo wa taifa letu kiuchumi ambao ndiyo huamua uwezo wa Serikali kifedha kukidhi mahitaji ya wafanyakazi ndiyo mambo yanayoturudisha nyuma. Kwa sababu hiyo, hatuwezi kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kiwango tunachokitaka sote. Pamoja na hayo katika miaka sita iliyopita, karibu kila mwaka tumechukua hatua za kuboresha maslahi ya wafanyakazi. Leo narudia kuahidi kuwa tutaendelea kufanya hivyo hata mwaka huu.
Ndugu Wafanyakazi;
Katika miaka sita hii, tumeendeleza juhudi za kukusanya mapato ya Serikali na tumefanikiwa sana. Mapato ya Serikali yameongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 125 kwa mwezi hadi shilingi bilioni 433 kwa mwezi au kutoka jumla ya shilingi trilioni 1.9 mwaka 2005/6 hadi shilingi trilioni 5.2 mwaka 2010/11. Mwaka huu tunaelekea kufanikiwa zaidi. Katika kipindi cha Julai hadi Machi 2012 tumefikia shilingi trilioni 4.8 ambayo ni sawa na asilimia 102 ya lengo la makusanyo kwa kipindi hicho.
Kwa sababu ya mafanikio hayo tumeweza kuongeza kima cha chini cha mshahara Serikalini kutoka shilingi 65,000 kwa mwezi mwaka 2005 hadi shilingi 150,000 mwaka 2011. Kwa nyongeza hizo za mishahara, katika mwaka huu wa fedha Serikali inatarajia kutumia jumla ya shilingi trilioni 3.2 kati ya shilingi trilioni 6.7 za mapato ya ndani kwa ajili ya mishahara. Hii ni asilimia 48 ya mapato hayo. Mishahara huchukua sehemu kubwa ya kiasi hicho cha mapato ya Serikali, hilo ndilo jambo linalokuwa kikwazo katika kuongeza mishahara na maslahi mengine ya wafanyakazi kama ambavyo sote tungependa iwe. Vinginevyo, pesa kwa ajili ya kutoa huduma muhimu kwa wananchi na kwa utekelezaji wa majukumu ya kiutawala, kiuchumi, na ya ulinzi na usalama ya Serikali yatakwama. Kwa sababu ya kutaka tuwe na uwiano mzuri, ndiyo maana tumekuwa tunaongeza mishahara kidogo kidogo kila mwaka.
Wakati huo huo tumekuwa tunaongeza juhudi za kuongeza mapato ambapo, kama nilivyokwishaeleza kwamba tunazidi kupata mafanikio. Kwa ajili hiyo, tunaendelea kutekeleza mikakati ya kupanua wigo wa walipa kodi na kuzidi kubana mianya inayovujisha mapato ya Serikali. Aidha, tunaangalia upya misamaha ya kodi. Mwaka wa jana kwa mfano, misamaha ya kodi ya kisheria ilifikia shilingi trilioni 1.05. Tumeamua kuzitazama upya sheria husika ili tuone wapi tunaweza kupata nafuu na kuiongezea Serikali uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa wananchi pamoja na wajibu wa msingi wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi wake.
Mfumuko wa Bei
Ndugu Rais wa TUCTA na Ndugu Wafanyakazi;
Nakubaliana nanyi kwamba katika hali hii ya ujira na maslahi yasiyotosheleza mahitaji, mfumuko wa bei unafanya maisha ya wafanyakazi kuwa magumu. Napenda kuwahakikishia kuwa tatizo la mfumuko wa bei tunalitambua na kwamba Serikali imekuwa inachukua hatua mbalimbali kudhibiti mfumuko wa bei na kupunguza makali yake. Bila ya juhudi hiyo pengine hali ingekuwa mbaya zaidi.
Lazima niwe mkweli kwamba siyo kazi rahisi hata kidogo. Kwa nini nasema hivyo? Kinadharia mfumuko wa bei unatokana na ujazi wa fedha kuwa mkubwa mno kuliko bidhaa. Mara nyingi Serikali kukopa sana kutoka katika mabenki huwa ndicho kichocheo katika mazingira hayo. Hapa nchini hilo silo tatizo na hata kama lingekuwa, ingekuwa rahisi kuudhibiti kwa kutumia sera za fedha na bajeti. Kiini cha mfumuko wa bei hapa kwetu ni kupanda kwa bei za nishati ya mafuta na umeme na kupanda kwa bei za vyakula.
Bei ya mafuta imepanda huko tunakoyanunua na hivyo kusababisha gharama ya kila shughuli inayotumia mafuta hapa kwetu kupanda. Kwa sababu hiyo, gharama za usafiri na uchukuzi, uzalishaji umeme, uzalishaji viwandani na mashambani pamoja na mafuta ya matumizi ya majumbani na kwingineko zimepanda. Hivyo basi, kuongeza gharama ya maisha kwa watu wanaotumia bidhaa na huduma hizo.
Kwa upande wa umeme, juhudi zetu za kuongeza uzalishaji wa umeme kutokana na gesi asilia utatupunguzia mzigo huo katika muda wa kati na mrefu ujao. Kwa upande wa bei ya mafuta hatuwezi kutabiri hali hii itakuwaje huko mbele ya safari hasa baada ya mwezi Julai wakati vikwazo dhidi ya mafuta ya Iran vitakapoanza kutekelezwa kwa dhati na nchi za Ulaya na Marekani.
Kwa upande wa bei ya chakula kuna sababu kadhaa. Ipo ile inayochangiwa na kupanda kwa bei ya mafuta, hivyo kupandisha gharama za uzalishaji na uchukuzi wa mazao kuyafikisha kwenye masoko. Lakini katika miaka ya hivi karibuni mvua kutokunyesha kwa kiwango cha kuridhisha na kwa mtawanyiko usiokuwa mzuri, kumesababisha kupungua kwa uzalishaji wa mazao na kusababisha upungufu wa chakula.
Ndugu Wafanyakazi;
Kana kwamba hilo halitoshi, nchi jirani nazo kutegemea nchi yetu kupata chakula chao kumelifanya tatizo kuwa kubwa zaidi na kusababisha bei za mahindi, mchele, sukari na maharage kupanda sana.
Mwaka wa jana niliagiza Wakala wa Chakula wa Serikali (NFRA) waanze utaratibu wa kuuza chakula mijini hasa nyakati za upungufu wa chakula kinacholetwa katika masoko kutoka vijijini. Lengo langu katika kufanya uamuzi ule ni kutaka kusaidia kupunguza makali ya bei ya vyakula mijini na hivyo kuwapa nafuu wakazi wa mijini na hasa wafanyakazi. NFRA wameanza kuuza chakula mijini lakini bado mpango huu haujafanikiwa vya kutosha. Nimeagiza wabaini upungufu uliopo na kuurekebisha ili uwe ukombozi kwa wakazi wa mijini.
Kwa upande wa sukari na mchele tuliwaruhusu wafanyabiashara binafsi kuagiza bidhaa hiyo toka nje bila kulipa ushuru wa forodha (Surchage). Waliopewa vibali wamekuwa wanaleta sukari lakini sijaridhishwa na kasi ya uagizaji. Naambiwa wapo watu walioomba vibali ambao uwezo wao ulikuwa mdogo na hivyo kuwanyima Watanzania fursa ya kunufaika na vibali hivyo na nafuu ya kodi. Nimeagiza Wizara husika zifanye ukaguzi wa utekelezaji wa waliopewa zabuni ili wale walioshindwa wanyang’anywe na kupewa watu wengine wenye uwezo.
Pamoja na hatua hizo tumefanya uamuzi wa makusudi wa kuongeza uzalishaji wa mpunga na sukari nchini. Kwa upande wa sukari tayari hekta 80,000 zimeshatambuliwa kwa ajili ya kulima mashamba na kujenga viwanda vya kuzalisha sukari. Kazi ya kutambua maeneo zaidi katika Bonde la Rufiji na mabonde mengine nchini inaendelea. Aidha, juhudi zinaendelea za kutafuta wawekezaji wa kutoka ndani na nje kuwekeza katika uzalishaji wa sukari. Kwa upande wa mchele, mikakati inaendelea ya kupanua na kuboresha uzalishaji wa mpunga katika mabonde kadhaa hapa nchini. Kwa kuanzia nguvu zetu tumezielekeza Wilaya ya Ulanga na Kilombero.
Kodi Kubwa
Ndugu wafanyakazi;
Kilio chenu cha kupunguziwa kiwango cha kodi ya mapato tumekipokea kwa uzito unaostahili. Jambo hili si geni. Mlishalileta siku za nyuma na tumechukua hatua na tunaendelea kuchukua hatua. Mwaka 2007 tulipunguza PAYE kutoka asilimia 18.5 hadi asilimia 15 kwa lengo la kuwapunguzia mzigo wafanyakazi wa kipato cha chini. Aidha mwaka 2010/11 tulipunguza kodi hiyo kutoka asilimia 15 hadi 14, sambamba na kuongeza kima cha chini cha mshahara kisichokatwa kodi kutoka shilingi 100,000 hadi kufikia shilingi 135,000. Serikali itaendelea kupunguza kiwango cha kodi hatua kwa hatua ili kuwapunguzia wafanyakazi mzigo wa kodi.
Vilevile tutaendelea kubuni njia mbalimbali za kuwafikia watu wengi zaidi waliopo nje ya mfumo wa kulipa kodi ili walipe na kuwapunguzia mzigo wa kodi kwa wafanyakazi. Naamini mpango wa kutoa vitambulisho vya taifa utakapotekelezwa kwa ukamilifu, utasaidia kutambua walipa kodi wengi ambao hivi sasa hawajajulikana.
Ukosefu wa Ajira
Ndugu wafanyakazi;
Nchi yetu, kama zilivyo nchi nyingi duniani inakabiliwa na tatizo kubwa la ajira hasa kwa vijana. Ukosefu wa ajira hapa nchini umefikia karibu asilimia 12 kwa mujibu wa sensa ya kazi ya mwaka 2006. Taarifa ya Utafiti ya Shirika la Kazi la Kimataifa (ILO) inaonyesha kuwa mnamo mwaka 2011 watu wapatao milioni 200 hawakuwa na ajira duniani, na inategemewa kwamba idadi hiyo itaongezeka na kufikia watu milioni 204 mwaka huu (2012) na ifikapo mwaka 2013, idadi hiyo itafikia watu milioni 209.
Kwa kutambua umuhimu wa kuchukua hatua thabiti za kukuza ajira ili kupunguza tatizo hilo, Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2005 ya CCM iliipa Serikali yake lengo la kuzalisha ajira milioni moja. Bahati nzuri lengo hilo liliweza kufikiwa na kuvukwa. Ajira milioni 1.2 zilizalishwa. Katika kipindi hiki Serikali imejipanga kuzalisha ajira maradufu ya zile za kipindi cha kwanza.
Kwa ajili hiyo hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa ili kuzalisha ajira mpya nyingi zaidi. Niruhusuni nitaje baadhi tu ya hatua zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa:
1. Tumefanya maboresho katika kuendeleza rasilimali watu hasa katika nyanja za elimu, mafunzo na ujuzi ili kuwawezesha wahitimu wake wawe na sifa za kuajiriwa ndani na nje ya nchi na uwezo wa kujiajiri wenyewe. Tumeelekeza kuwa mitaala ya shule na vyuo izingatie kutoa elimu na mafunzo yanayotakiwa na soko la ajira. Kadhalika vijana wapate elimu na mafunzo yatakayowawezesha kujiajiri. Kwa ajili hiyo tumesisitiza somo la ujasiriamali kufundishwa shuleni na vyuoni. Hii itawawezesha vijana kujua namna ya kuanzisha na kuendesha shughuli za uzalishaji na huduma zitakazowapatia mapato.
2. Tumeanza kuchukua hatua za kutekeleza mkakati maalum wa kuwatafutia Watanzania ajira nchi za nje. Hatua hizo zimewezesha vijana wa Kitanzania 1,327 kupata ajira katika nchi za Oman, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu kupitia Wizara ya Kazi na Ajira katika mwaka 2011/12. Lengo letu ni kuona vijana wengi zaidi wanapata ajira katika nchi hizo na nyinginezo nyingi duniani kama walivyo majirani zetu.
3. Kwa nia ya kuwasaidia vijana kupata ajira hapa nchini, tumeamua kuunda Kamati Maalum za kukuza ajira katika kila Wizara na Mikoa. Kwa kuanzia Wizara sita na Halmashauri 12 katika mikoa ya Lindi na Mtwara zimeunda Kamati Maalum na madawati ya kukuza ajira. Wizara hizo ni pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Fedha, Wizara ya Ujenzi pamoja na TAMISEMI.
4. Tumeendelea kuwawezesha wajasiriamali wadogo wa Tanzania kushiriki katika maonyesho ya kila mwaka ya nguvu kazi/jua kali ya nchi za Afrika Mashariki. Lengo letu kuu ni kuwapatia wajasiriamali wetu wadogo (ambao ndio wengi) fursa ya kujifunza, kupata soko na kutumia fursa hizo kukuza shughuli zao wazifanyazo. Kwa kufanya hivyo, Watanzania watanufika na fursa za itifaki ya soko la pamoja la Afrika Mashariki. Wastani wa wajasiriamali 106 wamekuwa wakiwezeshwa kushiriki maonesho husika (Nguvu Kazi/Jua kali) kila mwaka kwa kipindi cha miaka 13 sasa.
5. Kupitia mradi wa kujenga usawa wa jinsia na ajira bora kwa wanawake, hadi kufikia mwezi April 2012 kiasi cha shilingi bilioni 1.23 kimekopeshwa kwa wanawake. Wanawake wapatao 4,097 wamenufaika kupitia SACCOS za wanawake katika wilaya za Kinondoni, Ilala, Temeke na Tukuyu. Baada ya mafanikio yaliyopatikana katika Wilaya hizo, tunajipanga kueneza mpango huu nchi nzima.
6. Mtakumbuka kuwa mwaka 2006 tulianzisha Mfuko wa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo. Tulitenga shilingi bilioni moja kwa kila mikoa ya Tanzania Bara na shilingi milioni 200 kwa Mjini Magharibi na shilingi milioni 100 kwa mikoa mingine minne ya Unguja na Pemba. Kwa upande wa Tanzania Bara, hadi kufikia mwezi Desemba, 2010, ilitolewa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 47.3 kwa wajasiriamali 73,496, SACCOS 192 na vikundi vya kiuchumi 86. Wote hao wamejiajiri na kuwawezesha watu kadhaa kupata ajira. Tumekamilisha tathmini ya mpango huu na makakati unaandaliwa wa kuuendeleza. Shabaha yetu ni kuongeza fedha na kuboresha mfumo wa ukopeshaji, utafutaji na usimamizi wa wakopaji.
7. Serikali imeendelea kuwekeza katika shughuli za ujenzi wa majengo na miundombinu, shughuli ambazo zimekuwa zikitoa ajira nyingi kwa wananchi. Katika miaka ya 2009, 2010 na 2011 peke yake shughuli hizi zimepanuka sana. Jumla ya miradi mikubwa 8,870 yenye thamani ya shilingi trilioni 7.6 ilisajiliwa na Bodi ya Wakandarasi. Miradi hii imezalisha ajira 59,743 kati ya mwaka 2010 na 2012 kwa wahandisi na wataalamu wa fani mbali mbali, mafundi, vibarua, wenye magari ya uchukuzi, madereva na waendesha mitambo, mama lishe, wauzaji wa vifaa vya ujenzi, na watoa huduma za ujenzi.
Uwekezaji uliofanywa katika sekta ya ujenzi sio tu umeongeza ajira bali pia umeongeza mzunguko wa fedha nchini. Umesaidia kupunguza umaskini. Tutaendelea kuwekeza zaidi katika sekta hii ya ujenzi na sekta nyinginezo zenye kuzalisha ajira kwa wingi.
8. Tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo Serikali ilikuwa mwajiri mkubwa siku hizi ni sekta binafsi. Ni kwa sababu hiyo basi, Serikali inahimiza kukuza uwekezaji kutoka ndani na nje, na kuendeleza sekta binafsi ya wazawa nchini. Tumeendelea kuvutia uwekezaji katika Sekta ya Viwanda hususan kwenye Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZ) na Maeneo Maalum ya Mauzo Nje (EPZ). Mwaka wa jana peke yake, jumla ya miradi mipya 17 yenye thamani ya dola za Kimarekani 112 ilipatikana na kutoa ajira 8,059 kwa wananchi. Matarajio yetu kwa mwaka huu ni kupata miradi mipya 23 itakayozalisha ajira 14,500.
Maboresho katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii
Ndugu wafanyakazi;
Serikali inatoa umuhimu wa juu katika kuboresha maslahi ya wafanyakazi wakati wakiwa kazini na baada ya kustaafu. Sera na Sheria za Mifuko mbalimbali ya Hifadhi ya Jamii zina shabaha ya kuhakikisha kuwa mfanyakazi anapostaafu anaweza kuishi maisha mazuri. Tumetunga Sheria na kuanzisha Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA). Madhumuni ya mamlaka hiyo ni kuhakikisha kuwa, afya ya mifuko ni nzuri na inaendelea kustawi. Mamlaka hiyo imeanza kazi na kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha tathmini ya mifuko yote ya hifadhi ya jamii (Actuarial Valuation). Lengo la zoezi hilo ni kubaini maeneo ya kuimarisha na kuondoa tofauti za ukokotoaji wa malipo baina ya mifuko. Zoezi hili litakapokamilika litawasaidia sana wafanyakazi kujiandaa kustaafu na pia kupunguza makali ya maisha kwa wafanyakazi wanaostaafu, ili wastaafu kwa heshima.
Tija Kazini
Ndugu Wafanyakazi;
Pamoja na jitihada zote za kuongeza ajira, naomba tuendelee kukumbushana umuhimu wa wafanyakazi nchini kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kukuza tija kazini. Vyama vya wafanyakazi vinao wajibu mkubwa kwa hili kama walionao wa kutetea haki za wafanyakazi. Hakuna haki isiyokuwa na wajibu. Nawaomba wafanyakazi kutambua wajibu wa kufanya kazi kwa bidii, maarifa, uaminifu na uadilifu. Bado minong’ono ya Watanzania kutokufanya kazi kwa bidii na kutokuwa waaminifu ipo. Hali hii inawafanya baadhi ya wawekezaji wa kutoka nje na ndani kufikiria kuajiri wageni.
Nalirudia kulisemea jambo hili kwani si jema na kwamba tabia hii ikiendelea itafanya mazingira ya ajira kwa Watanzania kutokuwa mazuri. Nawasihi ndugu zangu tubadilike, ili watu duniani wapende kuajiri Watanzania. Inawezekana. Tunaweza kabisa kufanya kazi kwa bidii, maarifa, nidhamu, uaminifu na uadilifu. Haya shime tufanye hivyo na tuonekane tunafanya hivyo.
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu napenda kuzungumzia masuala matatu muhimu kwa taifa. Mawili nimekwishayazungumzia siku za nyuma na moja nalizungumza kwa mara ya kwanza. Jambo la kwanza ni Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika tarehe 26 Agosti, 2012. Duniani kote, nchi hufanya sensa kila baada ya muda wa miaka fulani; wengi hufanya kila baada ya miaka 10. Sababu na umuhimu wa sensa ni kuisaidia Serikali kupanga mikakati na mipango ya maendeleo ya nchi na maeneo kwa uhakika. Kwa kujua idadi ya watu na mtawanyiko wao ni rahisi kwa Serikali kupanga nini cha kufanya, wapi na namna gani. Nawasihi wafanyakazi na Watanzania wote kwa jumla mjitokeze kuhesabiwa siku hiyo. Si busara kukosa. Isaidie Serikali yako kupanga mipango ya uhakika kwa kuhesabiwa.
Katiba
Ndugu Wafanyakazi, Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ambalo ningependa kuliongelea siku ya leo ni Mchakato wa kupata Katiba Mpya ya nchi yetu. Wafanyakazi ni sehemu muhimu sana katika mchakato wa kupata Katiba mpya. Kama mjuavyo Tume ya Kukusanya Maoni ya Wananchi imeshaundwa na inaanza kazi zake rasmi siku ya leo. Baada ya muda si mrefu Tume itaelekeza utaratibu wa wananchi kutoa maoni. Narudia kuwaomba wafanyakazi na wananchi wote kwa jumla mjitokeze kutoa maoni yenu kuhusu Katiba ya nchi yetu. Ni fursa nzuri ya kutumia haki yenu ya kikatiba kutoa maoni yenu. Katiba ni kitu muhimu katika maisha na ustawi wa taifa na watu wake. Tafadhali jitokezeni msiache fursa hii ikapita halafu ukaja kulalamikia mambo yaliyomo katika Katiba mpya. Mwaka jana pale Morogoro mliomba kupata mwakilishi kwenye Tume ya Kukusanya Maoni ya Wananchi kuhusu Katiba. Hongereni kwa kupata uwakilishi katika Tume hiyo kupitia kwa Ndugu Yahaya Msulwa, Katibu Mkuu wa Chama Walimu.
Sakata la Bungeni
Ndugu Wafanyakazi;
Ndugu Wananchi;
Jambo la tatu ni mambo yaliyojitokeza katika Bunge lililopita. Katika Mkutano uliopita wa Bunge, taarifa ya mwaka wa fedha wa 2009/10 ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali pamoja na taarifa za Kamati za Kudumu za Bunge ziliwasilishwa na kujadiliwa. Mjadala wa taarifa hizo ndani ya Bunge na katika Kamati ya Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, ulikuwa mkali na mapendekezo kadhaa yalitolewa juu nini kifanyike kurekebisha upungufu uliobainika. Aidha, kumetolewa rai kwa baadhi ya Mawaziri kuwajibika au wawajibishwe. Katika jamii nako kumekuwepo na mjadala kuhusu taarifa hizo na yaliyotokea Bungeni. Kama ilivyo kawaida, kumekuwepo na maneno mengi na mengine ya uongo na opotoshaji kuhusu msimamo wangu na maoni yangu juu ya sakata la Bungeni. Napenda kuwahakikishia kuwa sikukasirishwa wala kufadhaishwa na mjadala wa Bungeni kuhusu taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Kinyume chake nimefurahi kwamba taarifa hiyo sasa inapewa uzito unaostahili na kwamba inajadiliwa kwa uwazi. Hayo ndiyo matakwa yangu. Narudia kuwapongeza Wabunge kwa jinsi walivyoijadili taarifa hiyo na mapendekezo yao. Tumejipanga vizuri kutekeleza mapendekezo yao.
Ndugu Wafanyakazi na Ndugu Wananchi;
Wanadamu husahau upesi. Mimi ndiye niliyefanya uamuzi kwamba taarifa za kila mwaka za ukaguzi wa hesabu za Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma ziwekwe wazi kwa wananchi kuzisoma na Bungeni zitengewe muda wa kutosha wa kujadiliwa. Kabla ya hapo taarifa hizi zilikuwa hazisikiki, hazionekani na wala hazizungumzwi. Hata Bungeni taarifa hizi zilikuwa ama hazizungumzwi au hazizungumzwi vya kutosha. Aghalabu huwekwa mezani tu na kama kuna mjadala basi huwa ni wa muda mfupi sana kwani kwa kawaida taarifa hizo hutolewa siku ya mwisho kabla ya hotuba ya kufunga Bunge. Kutokana na ushawishi wangu taarifa hiyo inapewa nafasi ya kutosha ya kujadiliwa.
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kuwa Rais mwaka 2005, (wakati wa kampeni) na baada ya kuwa Rais, (katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge la Tisa, 30 Desemba, 2005) nilielezea dhamira yangu ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kusisitiza nidhamu ya matumizi. Nafurahi kwamba kwa yote mawili mafanikio yanaonekana. Tumepata mafanikio makubwa kwa upande wa mapato ya Serikali kama nilivyokwishaeleza huko nyuma.
Kwa upande wa nidhamu ya matumizi nako tunaanza kuona mwanga wa matumaini ingawaje bado tunayo kazi kubwa ya kufanya. Katika mikakati yangu ya kufikia lengo hilo niliamua kwanza tuelekeze nguvu zetu katika kuimarisha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi. Hiki ndicho chombo kikuu cha kusimamia na kushauri kuhusu nidhamu ya matumizi ya fedha na mali za umma. Niliona bila ya kufanya hivyo kazi hii itakuwa ngumu sana au haitawezekana kabisa. Bila ya wao hutajua hali ikoje na hivyo huwezi kujua wapi pa kuanzia na nini kifanyike.
Baada ya kumteua Ndugu Ludovick Utuoh kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Septemba, 2006 nilimtaka jambo moja kubwa, nalo ni kuimarisha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ili tuweze kupambana na utovu wa nidhamu, wizi na ubadhilifu wa fedha na mali za umma. Lengo langu ni kutaka fedha na mali hizo zitumike kwa manufaa ya umma badala ya kunenepesha matumbo ya viongozi na watumishi wa Serikali wasiokuwa waaminifu na watovu wa uadilifu. Nilimuahidi ushirikiano na msaada wangu kwa yale atakayotaka Serikali ifanye kwa ajili hiyo.
Ndugu Utuoh alituletea Serikalini mahitaji yake na tumechukua hatua za dhati ambazo zimesaidia kuimarisha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi. Tumeiboresha Sheria ya Ukaguzi na kuiongezea mamlaka na kuihakikishia uhuru katika utekelezaji wa majukumu yake. Tumeiwezesha ofisi ya Taifa ya Ukaguzi. Tumeiongeza bajeti yake na hivyo wameajiri watumishi wengi wenye ujuzi wa kazi za ofisi hiyo. Wameongeza vitendea kazi kama vile, majengo ya ofisi Makao Makuu na mikoani, magari, computer n.k. Kazi ya kujenga na kuimarisha ofisi ya Taifa ya Ukaguzi tunaendelea nayo na inatupa moyo wa kufanya hivyo kwani matokeo yake kwa hapa tulipofikia ni mazuri.
Ndugu Wananchi ;
Baada ya kupokea taarifa yake ya kwanza ya ukaguzi, Machi, 2007, kusikiliza ufafanuzi wake na baada ya kuisoma na kuielewa nilitambua umuhimu na uharaka wa kuanza kuchukua hatua za kurekebisha mambo. Niliona tuanze na wahusika wanaozungumzwa katika taarifa hiyo. Nilitaka wasikie yale yanayosemwa juu yao kuhusu walivyotumia fedha na mali za umma. Kwa sababu hiyo, nilimtaka Ndugu Utuoh azungumze na Baraza la Mawaziri na Watendaji Wakuu wa Serikali. Tulifanya hivyo Dodoma. Baadaye niliwataka wazungumze na Wenyeviti, Wakurugenzi na Waweka Hazina wa Halmashauri za Wilaya na Miji. Niliitisha mkutano huo tarehe 28 Aprili, 2007 pale Ubungo Plaza.
Baada ya mikutano ya Ndugu Utuoh na Mawaziri na Watendaji wa Serikali Kuu na viongozi wa Halmashauri za Wilaya na Miji nchini, nilitoa maelekezo na maagizo kadhaa juu ya mambo ya kufanya kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha na mali za umma. Mosi, niliwataka viongozi na watendaji wakuu wa Wizara, Idara zinazojitegemea, Halmashauri za Wilaya na Miji na Mashirika ya Umma wazipe uzito unaostahili taarifa za ukaguzi kuhusu taasisi zao wanazoziongoza. Nilitaka wazisome na kuzijadili kisha wachukua hatua ya kurekebisha kasoro zilizoonekana.
Pili, niliagiza ziundwe Kamati Maalum za kuongoza na kufuatilia mwenendo wa mapato na matumizi ya fedha katika kila taasisi. Niliagiza kuwa Mawaziri waongoze Kamati za Wizara zao na wajumbe wake wawajumuishe Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Mhasibu Mkuu na Wakurugenzi au Makamishna waliopo Wizarani. Katika Halmashauri za Wilaya na Miji, Wenyeviti wa Halmashauri wataongoza kamati hizo na wajumbe wake ni Mkurugenzi Mtendaji, Mweka Hazina na Wakuu wa Idara. Kamati hizi pia zitajadili taarifa ya miezi mitatu ya Mhasibu Mkuu kabla haijapelekwa ngazi za juu.
Ndugu Wananchi ;
Jambo la tatu nililoagiza lifanywe ni kuwa, wahasibu wenye elimu na ujuzi stahiki wa mahesabu waajiriwe mapema iwezekanavyo na kupangiwa kufanya kazi katika Halmashauri zote nchini. Moja ya mambo ambayo Mkaguzi Mkuu alibainisha kwetu ni kuwa Halmashauri zina uhaba mkubwa wa wahasibu wenye ujuzi, jambo ambalo linachangia mambo kuwa mabaya. Kutokana na maagizo yangu hayo, wahasibu 795 waliajiriwa na kila Halmashauri ilipatiwa wahasibu wasiopungua watatu.
Ndugu Wafanyakazi na Ndugu Wananchi ;
Baada ya kuimarisha ukaguzi wa hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma, kuundwa na kufanya kazi Kamati Maalum na kuajiri na kusambaza Wahasibu wenye sifa, hali imeanza kubadilika na kuboreka. Hivi sasa Wizara na Halmashauri zinazopata hati zinazoridhisha (safi) zimeongezeka na zinazopata hati zisizoridhisha (chafu) zimepungua. Kwa mfano, mwaka 2009/10 taarifa ilikuwa kama ifuatavyo: Halmashauri zenye hati safi zilikuwa 66 hati zenye mashaka (qualified) 64 na hati chafu 4. Mwaka 2010/11 hali ilikuwa kama ifuatavyo: Hati zinazoridhisha 72, zenye mashaka 56 na zisizoridhisha 5. Hali kadhalika kwa upande wa Wizara nako kuna maendeleo ya kutia moyo. Taarifa ya mwaka 2009/10 inaonesha kuwa Wizara zilizopata hati zinazoridhisha 42, zenye mashaka 13 na zisizoridhisha 1. Taarifa ya Ukaguzi ya mwaka 2010/11 inaonesha kuna hati zinazoridhisha 50, zenye mashaka 10 na zisizoridhisha 0.
Ndugu Wafanyakazi na Ndugu Wananchi;
Kuna mambo manne mapya kuhusu ukaguzi wa hesabu za Serikali ambayo niliagiza yafanyike na sasa yanafanyika. Kwanza, kwamba, pamoja na ukaguzi wa vitabu vya hesabu vya taasisi, ufanyike ukaguzi wa thamani ya fedha (value for money) kwa yale yaliyoandikwa kuwa yamefanywa. Kazi hiyo sasa imeanza kufanyika, ndiyo maana hata Wahandisi ni wakaguzi katika Ofisi ya Taifa ya Mkaguzi. Katika baadhi ya maeneo au miradi, ukaguzi ulipofanyika mambo ya udanganyifu yamegundulika na wahusika kuchukuliwa hatua.
Jambo la pili ni kwamba, nilitaka CAG kutoa taarifa kwa vyombo vya kisheria pale atakapoona dalili ya wizi kufanyika. Kabla ya hapo, wajibu wa CAG ni kutoa taarifa kwa Rais ambaye nae huagiza Mawaziri husika kuziwasilisha taarifa hizo Bungeni. Hata kama amebaini wizi au ubadhilifu ni juu ya mamlaka husika. Niliona huu ni upungufu, tukarekebisha Sheria na sasa inafanyika.
Jambo la tatu ni ukaguzi wa uchunguzi (forensic audit) ambao shabaha yake ni kushauri taasisi kuhusu kasoro zilizopo au maeneo ya udhaifu ambayo yanahitaji kuimarishwa. Ukaguzi huo umeshafanywa Customs, NHIF na Halmashauri ya Misungwi kwa mfano.
Jambo la nne ni kuwa na Wakaguzi wa Ndani katika kila Wizara na Idara zinazojitegemea ambao wanawajibika moja kwa moja kwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali. Huko nyuma Wakaguzi wa Ndani walikuwa wanawajibika kwa Makatibu Wakuu wa Wizara na Wakuu wa Taasisi, jambo ambalo nililiona lingewafanya Maafisa hao kukosa uhuru wa kutosha kutekelekeza majukumu yao.
Ndugu Wafanyakazi na Ndugu Wananchi;
Nimeyaeleza haya yote kwa kirefu mjue tulikotoka, tulipo sasa na huko mbele tuendako. Nataka muelewe na kutambua jitihada tulizozifanya kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha na mali za umma. Lakini tumechukua hatua, tunaendelea na tutaendelea kuchukua hatua. Mafanikio yanaanza kupatikana lakini si ya kiwango cha kutufanya tufurahi sana. Bado tuna safari ndefu na kazi kubwa ya kufanya mbele yetu kwa sababu tumeanza katika hali ya chini sana. Mimi napata faraja kwamba muelekeo wetu ni mzuri na naamini tutafika pale tunapopataka, yaani “Mapato ya Serikali yataongezeka na fedha zinatumika kuwanufaisha walengwa“.
Hitimisho
Ndugu Wafanyakazi;
Nimeongea mengi. Ujumbe wangu mkubwa kwenu wafanyakazi wenzangu ni kuwa Serikali inatambua mazingira ya wafanyakazi na tuko tayari kuchukua hatua ya kuboresha hali hiyo kwa kadri ya uwezo wetu uliopo. Hatuwezi kusubiri uwezo uwe mkubwa. Tutaendelea kugawa kilichopo kupunguza makali. Tutaendeleza juhudi za kudhibiti mfumuko wa bei pamoja na changamoto zilizopo. Hatutasita kufanya yale yaliyopo kwenye uwezo wetu.
Naomba nimalizie kwa kuwashukuru tena kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika siku hii adhimu. Ni heshima kubwa kwangu. Ahsanteni sana. Nawatakia sikukuu njema.
Asanteni kwa Kunisikiliza.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!