Mbowe, Dk. Slaa wazodoana kikaoni
Wazee: Hatutaki sera za ukabila, fujo
Mikutano yake yasusiwa na wananchi
NA MWANDISHI WETU
MPASUKO uliojificha kati ya viongozi wa juu wa CHADEMA, umejitokeza hadharani, baada ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe kumshukia Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa.
Mbowe alimjia juu Dk. Slaa mbele ya kikao kilichohusisha viongozi wa mkoa na wilaya kutokana na tabia yake ya kuwatimua viongozi katika maeneo mbalimbali nchini.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho, kilichofanyika usiku wa kuamkia jana, katika ukumbi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), wilayani Ruangwa, mkoani Lindi, zilisema Mbowe alimshukia Dk. Slaa, akisema tabia yake imekuwa ikikwamisha utendaji wa chama hicho.
Kauli ya Mbowe ilitokana na Dk. Slaa kuwatimua baadhi ya viongozi, akiwemo Mwenyekiti wa wilaya na mlezi wa chama hicho, Hamis Lichonyoma, aliyewahi kuwa mwenyekiti wa mkoa wa chama hicho.
Imeelezwa kuwa viongozi hao waliitisha kikao kujadili mahudhurio mabaya katika mikutano ya chama hicho inayofanyika maeneo mbalimbali, kutokana na wananchi kuchoshwa na aina ya siasa zinazofanywa na CHADEMA.
Hata hivyo, kabla ya kuanza kwa kikao hicho, Dk. Slaa aliamuru kufukuzwa kwa baadhi ya viongozi kwa kile alichodai ni wasaliti, jambo lililomkera Mbowe.
Mbowe alitaka watendaji hao kuelekezwa namna ya kufanya kazi badala ya kufukuzwa, kwani kufanya hivyo ni kuendeleza migogoro ndani ya chama hicho.
“Hali ni mbaya katika mikutano yetu tunayoifanya kusini, wananchi hawataki kuhudhuria, hivyo kikao kilikuwa ni kujadili sababu.
“Bila kuangalia sababu kuwa wananchi wamechoka na siasa zetu, Dk. Slaa amekuwa akitimua viongozi kwa madai ni wasaliti, jambo ambalo si kweli,” alisema mmoja wa viongozi waliohudhuria kikao hicho.
Kiongozi huyo amefichua kuwa, katika baadhi ya maeneo wananchi wanashindwa kuitikia salamu yao ya Peoples Power (Nguvu ya Umma), jambo linalowafanya kuwafundisha kama vile hakuna wawakilishi wa chama hicho.
Chanzo hicho cha habari kilisema hilo limekuwa likiamsha hasira kwa viongozi wa juu wa CHADEMA, hivyo kuwatuhumu watendaji kuwa ni wahujumu.
Hata hivyo, imeelezwa Dk. Slaa aliendelea na msimamo wake, hivyo kuwatimua viongozi hao na kuweka safu mpya, kinyume cha maelekezo ya kiongozi wake.
"Ndani ya CHADEMA hakuna demokrasia, watendaji wemetimuliwa na kuwekwa wengine wanaowataka. Walikuwepo baadhi ya wabunge katika kikao na hawakusema lolote,” alisema.
Wakati mpasuko huo ukishika kasi, wazee takriban 200 wilayani hapa, wameitaka serikali kuendelea kuchapakazi na kamwe wasitishwe na kauli za CHADEMA.
“Tumewapa salamu kuwa hatuwataki, ndiyo maana hawaoni watu katika mikutano yao, serikali ya CCM iendelee kufanya kazi bila hofu, kwani kauli za CHADEMA ni sawa na ngoma ya watoto ambayo haiwezi kukesha,” alisema Ally Mayongola.
Wazee hao walitoa msimamo huo wakati wa mkutano kati yao na Naibu Waziri wa TAMISEMI (Elimu), Kassim Majaliwa, aliye ziarani wilayani hapa.
Mayongola alisema Ruangwa ni ngome imara ya CCM na kamwe CHADEMA haitapata nafasi ya uongozi katika jimbo hilo, kwani hawana sababu za kuwafanya wapewe uongozi.
Alisema wananchi wa Ruangwa hawako tayari kubaguana na kwamba, kukabidhi jimbo kwa chama kinachohubiri sera ya ukabila, udini na uvunjifu wa amani ni kuwapoteza.
“Tunashindwa kuelewa sababu za wao kuacha kusimamia maendeleo katika maeneo yao na kuja kupoteza muda huku.
“Wanazunguka nchi nzima kuhamasisha chuki na vurugu ili wananchi waichukie serikali, huu ni usaliti kwa wananchi waliowachagua ili wawaletee maendeleo,” alisema.
Source: GAZETI MOJA LA KILA SIKU
Kwa mtu anayefanya analytical politics hawezi kuwa manachadema..sisi ccm tuweke viongozi wanaokubalika na wananchi katika maeneo yao..hii ndo solution dhidi ya maeneo ccm iliyopoteza..