SERIKALI ya Finland imeahidi kuisaidia Tanzania kuharakisha kuandaa na kukamilisha mipango ya matumizi bora ya ardhi, vijijini.
Ahadi hiyo ilitolewa na Heidi Hantala ambaye ni Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa nchi hiyo alipofanya ziara yake ya kikazi wilaya ya Mufindi kukagua shughuli mbalimbali zinazopata ufadhili wa nchi yake.
Hantala aliyekuwa ameambata na Balozi wa Finland nchini, Simika Antila na maafisa wengine wa ubalozi huo na serikali yao alisema thamani ya ardhi inazidi kuongezeka siku hadi siku hivyo ni muhimu kila kijiji kikawa na mpango huo.
“Kila kijiji kikiwa na mpango huo, na kikiwa na hati miliki ya ardhi yake itawawezesha kuainisha mipango yenu ya maendeleo ipasavyo kwa kuzingatia kwamba matumizi ya ardhi yanaongezeka kutokna na shughuli za wananchi na zile za wawekezaji,” alisema.
Alisema kwa zaidi ya miaka 40 iliyopita serikali ya Finland imeendelea kuwa mbia mzuri wa maendeleo wa Tanzania hivyo haiwezi kuona shida kusaidia mipango hiyo.
Awali Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mufindi, Alli Kidwaka alimweleza waziri huyo na ujumbe wake kwamba kati ya vijiji 125 vya halmashauri hiyo, ni vijiji 58 vilivyokamilisha kuandaa mpango huo.
Alisema kasi ya halmashauri hiyo kuandaa na kukamilisha mipango hiyo ni ndogo kwasababu ya ukubwa wa gharama zake.
Kutokana na tatizo la fedha, Kidwaka alisema halmashauri hiyo inamudu kuandaa mpango huo kwa vijiji vinne tu kwa kila mwaka.
Alisema mpango wa matumizi bora ya ardhi ni mpangilio wa matumizi ya ardhi iliyoendelezwa na ambayo haijaendelezwa kwa faida ya wananchi na shughuli nyingine mbalimbali za kimaendeleo zikiwemo za uwekezaji.
Kabla ya kutoa ahadi hiyo, Waziri huyo alitembelea miradi mbalimbali katika sekta ya misitu, ufugaji na viwanda inayopata ufadhili wa nchi yake.
Miradi aliyoitembelea ni pamoja na ile Miradi ya Vikundi vya Wapandaji Miti kikiwemo kikundi cha Nundwe, vikundi vya wafugaji na Kiwanda cha Mbao cha Saohill.